Sep. 21, 2017

TABIA 100 ZINAZOCHANGIA KUUA HUDUMA [OVERCOMING 'CHURCH SHOPPING"]

Kanisa ni nini? Watu wa kawaida wanaposikia neno “kanisa” moja kwa moja hujenga dhana ya jengo la kanisa. Ni kweli jengo la kanisa linaweza kuitwa kanisa. Hata kamusi ya Webster inasema kanisa ni jengo la kuabudia wakristo. Lakini katika maandiko Matakatifu hatuoni mahali ambapo jengo la kanisa linaitwa kanisa. Kwa hiyo ni lazima tuwe na dhana ya kibiblia kuhusu kanisa.

Kanisa mahali hapa siyo jengo bali ni kutano la wakristo (yaani waliomwamini Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yao) na hukusanyika kuabudu pamoja. Au kwa lugha ya Kigriki ECLESSIA.

Tunaposema kukua kwa kanisa kuna aina mbili; kuna kukua kiidadi (Matendo 2:47ff), na kukua kiroho (yaani waumini hao wanafikia kiwango cha kuwa watu wazima kiroho). Ukuaji wa aina ya pili ni wa kidhahania sana, yaani kwamba si rahisi kujua kuwa huyu mtu amekua au la! Kwa sababu yule unayemdhani amekua kiroho, unaweza ukamshangaa akafanya jambo ambalo jamii nzima inashangaa na kusema “jamani, huyu siyo yule....” nk. Kwa hiyo basi ili kuondoa utata, katika makala haya nitazungumzia kukua kunakokadirika; yaani kukua kiidadi au kwa lugha nyepesi; kuongezeka kwa watu kanisani.

Kuhusu mchungaji

Kuna mafungu matatu katika Agano Jipya yenye neno "mchungaji" (kwa aina mbalimbali): Waefeso 4:11, Matendo 20:28, na 1 Petro 5: 2. Katika Waefeso 4:11, Paulo anazungumzia majukumu mbalimbali ambayo Kristo aliweka katika kanisa. Anatarajia "wachungaji na walimu" kutumikia kanisa. Maneno "wachungaji na walimu" huwatambua kama kundi moja.

Ni maana ya ujumla kwamba mchungaji ni mtu aliyeitwa na Mungu na kupewa jukumu maalum la kufanya kazi yake. Mchungaji ni lazima awe amepata uhakika na mwito wake kutoka kwa Mungu mwenyewe kulingana na maandiko matakatifu. Biblia inayo maelezo ya kutosha kuhusu sifa za mchungaji na mwito wake. Ama kwa hakika biblia haijasema kwamba mchungaji awe mkamilifu kabisa lakini ni lazima awe na uhakika na kile anachokifanya kama Biblia inavyoagiza.

Mtu anaweza kuthibitisha kwamba ameitwa na Mungu kutokana na uthibitisho wa ndani ya moyo wake. Yaani anakuwa na nia ya kufanya kazi ya uchungaji. Tunaweza kuchunguza kidogo andiko la 1 Timotheo 3:1-6 linalosema “ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.

Kulingana na andiko hilo tunagundua kuwa kumbe mchungaji lazima atamani kwanza kazi ya uchungaji. Huu ndio tunauita wito wa ndani mwako kwa vile Mungu alivyokuita. Halafu kuna uthibitisho kutoka nje, yaani inawezekana jamii inayokuzunguka (ya waamini); labda wachungaji wengine, au watu wanaodumu katika maombi, Mungu anaweza kuwatumia kukuambia kuwa wewe utakuwa mchungaji.

Ninao uzoefu katika jambo hili; mwito wangu wa nje nilipokea kutoka kwa mchungaji Wilson Bundala wa kanisa la AICT mwaka 1999. Nakumbuka kila mara tulipoonana naye aliniita jina “Mchungaji.” Wakati ule mimi sikujua kwa nini ananiita hivyo. Siku moja aliniambia ameona kuna kitu ndani yangu kinachomthibitisha kwamba mimi ninao mwito wa kuwa mchungaji. Na kweli imekuwa hivyo. Namkumbuka mzee Stanly Mihayo; huyu alikuwa mzee wa kanisa la AICT Masanga-Meatu. Mzee huyu wakati mimi nikiwa mdogo alipenda sana kuniita “Daniel Mtu wa Mungu” wakati mwingine aliniita “Daniel Mtumishi wa Mungu.” Maneno yake yalitimia baada ya mimi kuwa mchungaji.

Hata hivyo, kuwa mchungaji siyo kutaka jina la heshima, wala kutamani kuvaa kora shingoni, au kutaka kusalimiwa na waumini kwa heshima kubwa! La hasha! Kazi ya uchungaji ni mzigo ambao Mungu anakupa kwa ajili ya kuwatumikia watu wake. Siku hizi kila kukicha tunaona wachungaji wanaibuka, lakini cha ajabu wengi wao wamejaa tamaa ya fedha. Kwenye makanisa yao wanawakamua waumini wao kama ng’ombe wa maskini. Ni aibu kubwa kwa kanisa.

Unapokuwa umeamua kuwa mchungaji kutoka moyoni mwako, basi ujue kwamba umepewa mzigo mzito sana katika maisha yako yote. Kwa nini ni mzigo mzito? Ni kwa sababu Mungu anapokuwa amekuletea watu kwenye kanisa unalochunga, maana yake amekuamini kutunza roho zao kwa kuzilisha neno. Yaani kanisani kwako akija hata mtu mmoja unapaswa umlishe neno la Mungu kwa sababu Mungu amemtuma kwako. Usimchukulie poa muumini mmoja anapokuja kwako, Mungu amemleta kwako ili umsaidie.  

Kama mtu huyu hatalishwa sawasawa, anaweza kudumaa, na kuwa dhaifu kiroho na hatimaye kimwili. Na kwa sababu ya kukosa mizizi ya kiroho ndani yake, basi hubaki kama alivyo, hawezi kushuhudia wengine na wala hawezi kumkaribisha mwingine kuja kanisani.

Unaweza kushangaa mchungaji unakuwa na waumini hao hao, hawajawahi kumkaribisha mtu kuja kanisani kwao, na wala hawana mpanago wa kufanya hivyo. Hapo usitegemee kuongezeka kiidadi, utabaki nao hao hao,na pengine unaweza kujitia moyo kwamba hawa ndo Mungu amenipa. Kumbe kuna tatizo.

SABABU ZINAZOSABABISHA WATU WAHAMEHAME MAKANISA:-

Ukiachilia mbali kwamba siku hizi watu wamekuwa na masikio ya utafiti, yaani hawawezi kutulia sehemu moja, ni wazi kwamba kuna sababu zinazosababisha hayo yote yatokee! Kwa ujumla katika utafiti wangu nilioufanya tangu mwaka 2014 mpaka hivi leo. Hebu ngoja tuzitalii sababu hizi

1.Inawezekana kutokana na watu kukosa majibu ya ahadi walizoahidiwa kabla ya kuokoka

            Tangu zamani ni watu wachache sana wanaoenda kanisani pasipo kupitia changamoto nyingi katika maisha yao. Watu wengi wanaposikiliza mikutano ya injili na jinsi watumishi wa Mungu wanavyowaahidi kwamba ukimpokea Yesu kristo mambo yako yatakuwa safi. Sasa mara wanapokaa kanisani kwa muda wa mwaka mmoja wanaona hali zao zinazidi kuwa mbaya, basi huamua kuondoka.

            Tumesikia mara kwa mara katika mikutano ya Injili nyimbo kama vile “kwa Yesu ni tambarare” au kama ukimwamini Yesu leo “magonjwa yako yatapona yote kabisa, hutaugua tena kwa Jina  la Yesu” umaskini wako utaondoka leo hii, leo Bwana anaenda kufanya muujiza wa kuokota hela, leo kuna mtu atakuja kukulipia kodi, leo mchumba wako atakuja jioni kukusalimia, leo mumeo kama alikuwa hatoi hela ya matumizi anaenda kukuachia laki moja, leo maadui wako wote wanaena kuwa marafiki wako kabisa, ndani ya wiki hii unaenda kununua kiwanja na mwakani majira kama haya utaenda kujenga, mwakani majira kama haya wewe mama utakumbatia mtoto, hata kama huna mume Mungu anaenda kukupa mume muda huu” pamoja na ahadi  nyingine lukuki!

            Ahadi hizo hapo juu siyo kwamba Mungu hawezi kuzitimiza kwa makusudi yake. Hakuna jambo linamloshinda Mungu, katika kubadilisha historia ya binadamu. Lakini wakati wa kuzitoa ahadi hizi lazima tuangalie kwanza hitaji  la mwanadamu ni nini? Naamini kwamba hitaji la mwanadamu la kwanza ni kuwa na uhusiano wake na Mungu zaidi na zaidi. Kutokuwa na mali za hapa duniani haimaanishi kwamba uhusiano wetu na Mungu pia umeharibika. Tatizo kubwa la mwanadamu ni dhambi inayomsumbua usiku na mchana, hilo tatizo likitibiwa vizuri mambo mengine anaweza kuvumilia hata pale yanapokuwa magumu.

            Ninachojaribu kusema hapa ni kwamba kwa sababu ahadi hizo zinaweza kushindikana kutimizwa mapema kwa majira ambayo mtumishi alisema, lakini pia kwa majira ambayo huyo aliyeahidiwa aliyapanga, na kwa kusahau majira ya Mungu; watu kama hawa hujikuta wakihamia sehemu nyingine ili kusaka ahadi zao, labda pengine Mungu wa mahali hapo hajatimiza haja za mioyo yao.

            Watu kadha wa kadha walipohamia kanisani kwetu niliweza kuwadadisi ni kwa vipi wamehama sehemu walizokuwa wanasali na kuamua kujiunga na huduma yetu. Mara kwa mara walinijibu sababu tofauti kama vile; kanisa lile liko hivi na hivi, lakini baada ya muda kupita waliondoka pia kanisani, kwa sababu hiyo niligundua shida yao nini hasa. Nilikugundua kwamba wanatafuta majibu ya maisha yao ya kimwili, lakini kwa sababu hawakuwa wawazi zaidi ndiyo maana wameondoka tena na kuelekea sehemu nyingine ili wakajaribu upya wa huko.

            Hivyo basi, mtumishi wa Mungu unapoona watu wanaanza kuondoka kanisani na kuelekea kanisa lingine, haijalishi wewe uko katika kiwango gani, hao bado hawajapata majibu ya maswali yao au zile ahadi walizoahidiwa siku ya kumpokea Bwana Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yao. Hili nalo wewe kama mtumishi wa Mungu liweke kwenye kumbukumbu kwamba lazima ugundue hitaji la mioyo yao na ahadi walizoahidiwa mara ya kwanza ni zipi.

by Daniel John Seni

______________________________________

kumbuka kitabu hiki kina sababu 100 zinazosababisha washirika wahamehame makanisani na kusababisha huduma kudumaa na hatimaye kufa

kama unapenda kuendelea kusoma kitabu hiki kwa mfululizo "andika hapa chini"