TITLE: KUSHINDWA KUPAMBANA ILI KUPATA BARAKA ZA KIMWILI NI UZEMBE AU MPANGO WA MUNGU?

TITLE: KUSHINDWA KUPAMBANA ILI KUPATA BARAKA ZA KIMWILI NI UZEMBE AU MPANGO WA MUNGU?

TEXT: MWANZO 49:3-4

UTANGULIZI: Unaweza kujiuliza, kwa nini nijifunze habari hizi? Hasa mimi ambaye ninaamini katika “predestination” ya Mungu, kwamba Mungu amekwisha kunichagua kwa ajili ya uzima wa milele na kwa namna moja au nyingine siwezi kupoteza nafasi yangu. Swali la kizushi, je inawezekana kupoteza nafasi yako ya mbinguni? Absolutely not! Lakini kuna vitu vingine kama vile baraka za kimwili za hapa duniani tunaweza kuzipoteza kwa sababu tunahitaji kufanya mambo fulani fulani kwa ajili ya kuzipata. Baraka pekee ambayo huifanyii kazi (hata hivyo unahitaji kuamini) ni ile ya kupokea uzima wa milele-lakini hizi zingine ni lazima tuwajibike na kwa nguvu zote ili tuzipokee.

Tukianza kuzungumza kwa habari ya Yakobo, hebu cheki alivyokuwa anakomaa kupokea baraka za hapa duniani. Ingawa Mungu alikuwa ameahidi kumpa baraka lakini ilibidi apambane kwa kadri iliwezekanavyo ili aweze kuzitwaa.

a)     Kwanza alinunua (kwa hila) baraka ya kaka yake ya uzaliwa wa kwanza. Mwa. 25:29-34, 27:36

b)     Pili alipambana na malaika wa Bwana na akamwambia kwamba usiponibariki, sikuachi (Mwa. 32:26-28

Kumbuka: ingawa ilikuwa ni ahadi ya Mungu kumbariki Yakobo na uzao wake (hata kabla hajazaliwa) lakini ilibidi apambane kwa ajili ya kuzipata baraka hizi.

Lakini mtu anapokuwa ameshindwa kuzipata zile baraka ambazo zimeelekezwa kwake kama mzaliwa wa kwanza, kuna wakati mwingine ni uzembe lakini wakati mwingine inakuwa imekusudiwa iwe hivyo, lakini uwajibikaji utabaki kuwa kwa mwanadamu mwenyewe kwa sababu yeye ndiye mhusika.

 1. MAISHA YA RUBENI KAMA MZALIWA WA KWANZA WA YAKOBO.
 • Katika fungu tulilosoma leo la Mwa.49:3-4 tunamuona mzee Yakobo anaanza kuwaabariki watoto wake kila mtu baraka ambayo ilimfaa (Mw.49:28).
 • Hapa tunakutana na mtiririko wa baraka kuanzia kwa mzaliwa wa kwanza mpaka kwa mzaliwa wa mwisho.
 • Katika baraka hizi, mzaliwa wa kwanza hajatendewa kile ambacho alitakiwa apokee. Yakobo anatupatia sababu za kwa nini hajampa baraka hizo.

a)     Alikipandia kitanda cha baba yake. (yaani alilala na mke wa baba yake – suria (Mw.35:22). Kitendo hiki kilikuwa ni kibaya sana kwa mtoto kuchangia mwanamke na baba yake. Hata leo kuna jamii nyingi, za kiafrika ambapo hata hawala wa baba yako hupaswi hata kumuuliza swali lolote. Na kama ikitokea tamaa imekukamata-basi ujue unatafuta laana badala ya baraka. Tukisoma fungu hili hatuambiwi matokeo yake-lakini tukisoma sura ya 49 tunaona namna ambavyo Yakobo anaondoa ile baraka ambayo ilitakiwa iwe kwa Rebeni. Je baraka hii ilipelekwa kwa nani? Tusome 1 Nyakat 5:1-2 hapa tunaona vitu vifuatavyo:-

 1. Haki yake ya mzaliwa wa kwanza ilihamishiwa kwa Wana wa Yusufu (ili awape baraka hii ya mzaliwa wa kwanza, Yakobo alimwmbia Yusufu katika  Mw. 48:5-6, anawamilikisha hawa vijana wawili kuwa wa kwake (yaani anasema siyo wajukuu wake bali ni watoto wake-mjukuu hamiliki pamoja na watoto (watoto ndio wanamiliki) kama wewe ni mjukuu huna nafasi pale. Kwa hiyo, ndiyo maana Yakobo aliwamiliki vijana hawa wawe wa kwake kwanza.
 2. Lakini vijana hawa hawakuwa na nguvu ya kutosha miongoni mwa Wana wa Israel. Turudi kwenye fungu la Nyakati anasema kuwa “lakini Yuda alikuwa na nguvu miongoni mwa ndugu zake” (1 Nyak.5:2). Ukisoma hapa unaelewa nini? Turudi kwenye Mw. 49:8 “Yuda ndugu zako watakusifu…fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda

Kwa hiyo kulingana na mafungu tuliyosoma yanatuonesha wazi kwamba Rubeni alishindwa kumiliki baraka za uzaliwa wake wa kwanza, kwa sababu ya makosa yake mwenyewe. Kana kwamba haitoshi hebu ngoja tulinganishe kati ya Reben na Yuda.

Wakati walipoenda nchini Misri kwa ajili ya kutafuta chakula. Yusufu aliwaambia kwamba hatauona uso wao pasipo kumleta mdogo wao wa mwisho (Benjamini). Wakati wanajaribu kumshawishi mzee Yakobo kwa ajili ya kumwachilia Benjamini aende pamoja nao, unaweza kugundua vitu kadhaa hapa. Ngoja tulinganishe kama ifuatavyo:-

 1. 1.     Rubeni alimwambia baba yake kuwa kama asipomrudisha Benjamini “waue watoto wangu wawili” (Mwa.42:37). Unafikiri Yakobo angekubali hoja hii? Yaani kwamba Yakobo awaue wajukuu wake wawili kwa ajili ya kufidia Benjamini. Tunaweza kujifunza mambo yafuatayo katika fungu:-
 • Rubeni hakufikiri juu ya watoto wake bali alifikiri yeye mwenyewe tu. Kwa sababu kama angefikiri juu ya watoto wake- na pia bado ni wajukuu wa mzee Yakobo asingesema hivyo.
 • Lakini kuweka watoto wako rehani kwa ajili ya kuuawa na babu yao ni dhambi. Kwani Mungu tayari alikuwa ameshasema kwamba atakayetoa uhai wa mtu uhai wake utadaiwa mikononi mwake. Kwa hiyo Rubeni hakutii hata agizo la Mungu.
 • Rubeni hakukumbuka siku ile mzee Yakobo alipowakemea watoto wake wawili (Simoni na Lawi) walipowaua wale watu wa Shekemu baada ya kumbaka Dina (dada yao) na ndiyo maana hata wakati wa baraka aliwaondolea baadhi ya vipengele muhimu kwa baraka zao.
 • Kwa hiyo hapa tunaweza kupata picha halisi ya Rubeni kama mzaliwa wa kwanza wa Israel
 1. 2.     Yuda alikuwa mtoto wa nne wa Israel kwa Lea (mke wake wa kwanza). (Mwa.29:35). Sasa hebu angalia yeye alivyombia baba yake katika  Mwa. 43:8-9
 • Alimhakikishia baba yake kwamba atamrudisha mtoto  na akajiweka dhamana yeye mwenyewe.
 • Alikubali kuchukua lawama juu ya maisha yake yote kwa ajili ya kuokoa familia nzima ipate chakula kwa sababu mzee Yakobo alikuwa amegoma kabisa.
 • Kupitia maombi ya Yakobo tunaona kwamba mzee Yakobo anakubali kuwapa kijana Benjamini aende pamoja nao
 • Yuda alikuwa tayari kubeba ile lawama (Mwa. 44:33)

Kwa hiyo kupitia mafungu haya tunaweza kuona kwamba ilikuwa ni HAKI kwa Yuda kupokea baraka za UKUU (ingawa hazikuelekezwa kwake) lakini moja kwa moja alizipokea kulingana na vitu alivyokuwa anavifanya kwa wakati huo. Moyo wa Rubeni ulimfanya kupoteza baraka za kimwili.

Umejifunza nini katika somo hili?

a)     Tunahitaji  kupambana katika kupata baraka za kimwili na wala tusimsingizie Mungu

b)     Mungu tayari ameshatupa baraka zake-ni kazi yetu kuchukua baraka hizo

c)     Kona kona nyingi katika maisha (uzembe pamoja na mambo mengine-tabia mbaya pia) vinaweza kusababisha kupoteza baraka za kimwili na kubaki na baraka za kiroho tu ambazo ni uzima wa milele. Yakobo alikuwa ana-struggle katika maisha yake kwa sababu alijua namna ya kuchukua baraka za Mungu za Kimwili. Labda nikwambie kwamba usimwombe Mungu kitu pale ambapo unajua kitu cha kufanya kwa sababu kama unajua kitu cha kufanya –basi ujue ni Mungu huyuhuyo ndiye aliyekupa wazo la kufanya na labda kama utaingiwa na kusitasita ambapo tena kusitasita hakuna imani. Kwa mfano; Je unaweza kuuliza njia ya kwenda Tegeta wakati unaijua kabisa? Litakuwa jambo la ajabu sana. Ndivyo hivyo watu wengi huuliza njia kwa Mungu ili hali wameshajua cha kufanya.

d)     Moyo wa mtu ni muhimu sana (attitude). Kama moyo wake ukiwa na mawazo mabaya lazima yatajidhihirisha tu.

e)     Naamini pia kupitia somo hili umejifunza mambo mengi kuhusu Yuda na Rubeni. Mungu akubariki sana ili elimu hii ibaki kwako na ikusaidie kutumia mafungu haya kwa utukufu wa Mungu.