MBONA YAMEKUSHINDA?

TITLE: MBONA YAMEKUSHINDA?

TEXT: MATHAYO 14:28-31

Utangulizi: Leo ninataka kuzungumza nawe kuhusu kushindwa kwako katika mambo fulani fulani na kwa nini mambo hayo yanaonekana yanakushinda.

Yesu aliwaamuru (aliwalazimisha) wanafunzi wake waende ng’ambo nyingine wakati yeye alikuwa akiwaaga makutano. Wakati wa usiku aliondoka na kwenda kuwafuata wanafunzi kule walipokuwapo. Kuna shida kubwa imewapata wanafunzi wake baharini “chombo kilikuwa kinaatabika (14:24) kwa sababu upepo ulikuwa ni wa mbisho (against)! Baadaye Yesu akaenda kukutana nao akiwa anatembea juu ya maji, biblia inasema kwamba walifadhaika sana na kusema “ni kivuli (ghost), wakapiga mayowe” ya woga! Sasa Yesu akasema “Ni mimi, msiogope”

Shughuli inaanzia hapa, wakati Petro alipotaka kuthibitisha kwamba aliyekuwa akiongea naye ni Yesu kweli au la! 

PETRO ANATAKA KWENDA PALE YESU ALIPO

Ikiwa ni wewe niamuru (siyo niambie) nije kwako (mst 27), maana ya “amuru” maana yake ni “command” siyo ni kushurutisha si kwa ombi! Mtu anayeamru huwa ana mamlaka ya kufanya hivyo. Kiunganishi KAMA kinatafsiriwa kama “KWA KUWA” hivyo inakuwa “kwa kuwa ni wewe Bwana”

  1. Yesu akamwamru “njoo”. Hii kauli pia ni ya kuamrisha kwamba mtu huyu ana mamlaka. kwa kawaida watu wenye mamlaka hutumia maneno mafupi kama “kuja, njoo, kula, vaa nk” mtu asiye na  mamlaka kwa kawaida ataanza kwa kusema “samahani, tafadhali, naomba nk”. Lakini Yesu alimwamru Petro kwamba “njoo”
  2. Jambo hili lilikuwa kubwa sana kwa Petro kwa sababu aliweza kutembea, siyo mzaha alitembea juu ya bahari. Petro alikuwa anapenda sana kuwa karibu na Yesu Kristo, hata katika Yohana 21:7 tunaambiwa aliwahi kujitupa baharini na kumfuata Yesu Kristo (tusome hapo).

Attention: hata hivyo alitembea hatua chache tu kwa sababu Biblia inasema alianza kuzama!

Maswali: kwa nini alianza kuzama? Ni kwa sababu aliona mawimbi ya bahari na upepo? Kwani Petro alikuwa hajui kuogelea? Na kama alikuwa anajua kuogelea kitu gani kilichomsumbua mpaka akafikia hatua ya kuanza kuzama na kupiga kelele kwamba Yesu nisaidie?

  1. I.                KWA NINI ALIYOYAANZISHA YALIMSHINDA?

Unajua kwa nini ninasema kwamba aliyaanzisha mwenyewe? Ni kwa sababu wenzake walikuwa ndani ya ile mashua yao-lakini kimbelembele chake Petro ndicho kilifanya atoke kwenye mashua.

  1. 1.     Alipoteza mwelekeo wake (focus yake) kwa yule aliyekuwa amemwamuru atembee kwenye bahari.

ð      Alipokuwa ameanza safari ya kumwendea alikuwa anatembea vizuri tu, lakini alipoacha kumwangalia yule aliyekuwa amemwamru kwamba “njoo” alianza kuzama haraka sana

ð      Nafikiri pia alianza kufocus katika vitu vilivyokuwa baharini; “akaona upepo” (kumbuka upepo ule ulikuwa bado haujatulia-maana walikuwa wanahangaika na safari yao bila Yesu ndani ya mashua). Kwa hiyo alikumbuka namna upepo ulivyokuwa unawasumbua walipokuwa kwenye mashua-sasa sembuse na kwamba niko nje ya mashua!

ð      Lakini siyo upepo tu mbaya zaidi ni kwamba pia aliogopa. Kwa sababu aliruhusu hofu iingie ndani ya moyo wake napo alianza kuzama.

ð      Pamoja na uzoefu wake wote wa kuogelea ilibidi APIGE KELELE KWAMBA Yesu ili apate msaada.

Swali lingine? Kitu gani kilichomfanya Petro atembee kwenye maji? Maana kama tukijua kwa nini alianza kuzama basi kuna sababu pia iliyomfanya atembee juu ya maji. Kwa nini alitembea juu ya maji?

ð      Jibu ni kwa sababu ya IMANI aliyokuwa nayo kwa YULE ALIYEKUWA amemwamru atembee juu ya maji. (tunajua hilo kwa sababu Yesu alimwambia ewe mwenye imani haba, kwa nini uliona shaka!) kwa taarifa yako ni kwamba IMANI YA PETRO ILIKUWA KUBWA KULIKO WOTE hapo maana wao walikaa ndani ya mashua lakini angalau alitembe!

ð      Imani ya Petro ilikuwa ndogo kiasi cha chembe ya haradali (Mathayo 17:20) lakini ilikutana na msukosuko wa hofu na mashaka- basi akaanza kuzama.

ð      Kwa sababu ya imani- ilimwezesha kutembea pale ambapo wengine hawawezi kutembea isipokuwa Yesu peke yake.

Mpaka tumeona kwamba mambo yalikuwa yamemshinda Petro, hakuna na namna nyingine kabisa- unajua wakati mwingine alitafakari, kwa dakika sekunde moja lazima niamue vizuri hapa.

Kwa mfano: dereva wa gari anapokuwa katika mazingira hatari-maamzi yake yanahitajika ndani ya sekunde moja awe ameshaamua. Akichelewa kuamua inaweza kusababisha bonge la ajali. Sasa Petro naye ilibidi ajikague kwa sekunde moja na kufanya maamuzi.

Labda pengine

a)     Alitafakari kwamba arudi kwa wanafunzi-maana mashua ilikuwa bado karibu naye-lakini bado angerudi kule kulikuwa na shida tu maana upepo ulikuwa ni wa mbisho tumeshasoma. Lakini pia kurudi kwa wale wanafunzi pengine wangeanza kumcheka tu na kumzomea vipi rafiki!

b)     Labda alitafakari uzoefu wake wa zamani wa kuogelea-kwamba hivi, hapa siwezi kupiga mbizi kweli? Lakini napo jibu likawa hapana maana mziki wa upepo ule haukuwa kawaida! Sasa nifanye nini? yaani haya maswali lazima yawe yalitukia ndani ya sekunde mbili, mara tu alipogundua kwamba ameanza kuzama. (maana kugundua kwamba ameanza kuzama nayo ni ishu ya msingi sana, maana unaweza ukawa unazama lakini hujielewi kama unazama.

Maamuzi yake yalikuwa sahihi:-

a)     Alisema Bwana NIOKOE (mst 30)

b)     Yesu akamwokoa na pamoja

c)     Walipopanda kwenye mashua “upepo ulikoma”. Tunaweza kujiuliza maswali kwamba kwa nini Yesu hakutaka kuendelea na safari ya majini pamoja na Petro na iliwabidi waingie tena ndani ya mashua? Labda tunaweza kusema kwamba muujiza ni TUKIO la muda na kwa makusudi maalum,lakini Mungu ameshatengeneza kanuni ya maisha ya binadamu si kutembea juu ya maji (samaki wafanyaje sasa)

APPLICATION

Sasa umeshaona kwa nini mambo yanakushinda?

a)     Ni kwa sababu unafocusi sehemu nyingine kuliko kumwangalia yeye aliyekuita

b)     Ni kwa sababu unaangalia hali ya maisha yako- ndio maana maisha yanakuwa magumu sana badala ya kumwangalia Yesu Kristo

c)     Ni kwa sababu pia wewe wakati mwingine unawaangalia wanadamu kana kwamba wanaweza kukusaidia kumbe hawawezi kabisa.

d)     Ni kwa sababu pia pengine wewe unaegemea uzoefu wako katika kutatua shida mbalimbali katika maisha yako, na ndiyo maana maisha yanaonekana kuwa ni magumu sana-kila siku unalalamika.

Ni wakati wa:-

  1. Kumwambia Yesu sasa kwamba “BWANA NIOKOE” eleza hali yako kama ulivyo bila kuficha mbele za Bwana. Yeye yuko mahali hapa kwa ajili ya kunyosha mkono wake akuinue tu.
  2. Biashara yako imeshaanza kuzama kabisa, madeni hayaishi, wateja huna, kila kitu hakiendi sawasawa-HEBU LEO TUSEME “BWANA NIOKOE MWENZIO NAKUFA”
  3. Biblia inasema kwamba “tumwangalieni Yesu Kristo peke yake” [Heb.12:2]. Yesu aliyeanzisha imani yetu atatuwezesha.
  4. Tumwangalie Yesu kwa imani kabisa. Kwa sababu imani ndiyo inayotufanya tusizame na maji ya duniani hii. Mungu akubariki sana.

Amen