TAREHE 21/5/2017

TITLE: UMEFANYA NINI ILI MUNGU AKUKUMBUKE?

TEXT: NEHEMIA 13:30

nikumbuke Ee Mungu wangu ili unitendee mema” (nikumbuke Mungu wangu kwa mema)

UTANGULIZI: Nehemia alikuwa nani? Ni mmojawapo wa Wayahudi waliokuwa wamepelekwa uhamishoni Babel. Huku wengine wakiwa wamesharudishwa Yerusalem, Nehemia akiwa katika nchi ya Babal alisikia habari mbaya kuhusu mji wa Yerusalem (1:10 na ndipo akaanza maombi maalum kwa ajili ya kufanya matengenezo ya 1) ukuta 2) ibada. Kupitia mambo haya aliyoyafanya ndiyo maana alipata kibali cha kumwambia Mungu amkumbuke. Tutakapokuwa tunajifunza utaona kama mara 4 hivi Nehemia anamwambia Mungu amkumbuke.

Mambo gani alifanya Nehemia?

Kazi kubwa aliyofanya Nehemia ilikuwa ni ya:

 1. I.                KURUDISHA HADHI YA TAIFA LA ISRAEL KATIKA NCHI YAO
 • Alisimamia ujenzi wa ukuta ingawa kulikuwa na upinzani mkubwa (4:1ff)
 • Maneno ya dharau kutoka kwa Wapinzani wake hayakumvunja moyo ( 4:3)
 • Wapinzani wake waliajiri mpaka manabii kumvunja moyo (6:10,14)

Matokeo: ukuta ulimalizika na watu wakakaa sehemu salama kabisa

App: inawezekana kabisa unapotaka kufanya kazi ya Mungu kwa namna yoyote ile maadui wanainuka. Wengine mpaka wanakutabiria mabaya kwamba huwezi kufanya jambo lolote! Simama na Bwana kwa imani kama Nehemia ambaye ama kwa hakika alisimamia kazi mpaka mwisho.

ð      Pengine wewe ni mwimbaji unataka kurekodi audio au video-hakuna hata mtu anayekutia moyo hata siku moja! Kila mtu anasema kwamba sauti yako ni mbaya na haifai, lakini wewe unajiona unaweza kuimba-komaa pasipo kuwasikiliza hao hawana lolote

ð      Pengine unayo huduma kanisani, kila unapotaka kufanya wapinzani wako wanakukatisha tamaa, mara wanakwambia “eti anajipendekeza ka mchungaji” wakikwambia hivyo-wewe endelea tu kwa sababu kazi ya Mungu inahitaji kujipendekeza pia ili tupate vibali kutoka kwa Mungu. Fanya huduma kutoka ndani ya moyo wako Mungu atakukumbuka tu usiwe na wasiwasi moyoni mwako.

ð      Wakati mwingine kila ukitaka kwenda kuhubiri nje watu wanakusema vibaya na kukuambia kwamba wewe hujui kuhubiri-komaa, Mungu anajua kilicho ndani yako

ð      Wakati mwingine yawezekana kabisa una mipango mizuri kwa ajili ya kurekebisha jengo la kanisa- lakini watu wanakukatisha tamaa-komaa, usiache kwa sababu ya maneno yao-Mungu atakukumbuka. Huhitaji kukumbukwa na wanadamu, kama Mungu akikukumbuka-inatosha kabisa.

ð      Nehemia aliguswa aliposikia ukuta wa Yerusalem umebomoka-na akatamani kuujenga-hebu leo wewe uguswe kwenye jengo la kanisa. Hebu mwambie Mungu aweke kitu ndani yako kama alichokuwa ameweka kwa Nehemia (tusome 2:12) kwa ajili ya nyumba ya Mungu. leo hii ndiyo siku nzuri kwako kwa kutoa ahadi ya kwamba utafanya nini kwa ajili ya nyumba ya Mungu leo. (mji wa Yerusalem)

 1. KURUDISHA HAKI YA NDUGU (KUKOMESHA UNYANYASAJI WA MASKINI) (5:1-19)
 • Maskini walikuwa na njaa lakini matajiri hawakutaka kuwapa chakula hata ndugu zao (5:2)
 • Kwa sababu ya kuwahurumia maskini, Nehemia hakutumia haki yake ya kupata chakula kama gavana (5:14-15, na hasa mstari wa 18)

Ndipo: akamwambia Mungu nikumbuke (5:19)

App: kuwakumbuka masikini katika shida zao ni mojawapo ya mambo ya muhimu katika maisha ya mkristo. Katika Yakobo tunaambiwa kwamba “dini iliyo safi ni kuwatazama wajane na yatima katika dhiki zao” (Yak.1:27) hii haimaanishi wajane tu na yatima ndio unapaswa kuwasaidia, mtu yeyote aliye maskini unapaswa kumsaidia. Pengine wewe una kampuni nzuri tu, lakini cha kushangaza badala ya kuwaajiri wapendwa-unatafuta watu wengine kwa nini? si vizuri hivyo-Biblia inasema ikiwa tuna nafasi tufanye mema kwa watu wote “hasa jamii ya waaminio”

 1. KURUDISHA IBADA YENYE HADHI MBELE ZA MUNGU
 • Aliliongoza taifa la Israel kutubu mbele za Mungu kwa ajili ya maovu yaliyopelekea kupelekwa uhamishoni Babel (9:1 hasa mstari wa 38)
 • Alirudisha hadhi ya watumishi wa Mungu makuhani kwa ajili ya kufanya kazi yao katika ibada (13:10) Walawi walisahauliwa na watu hawakupeleka zaka na matoleo mengine, na hivyo walawi waliondoka ndani ya nyumba ya Mungu na kwenda kwenye mashamba yao kujipatia chakula.

App: ndugu yangu mpendwa, mimi sikulazimishi kuwasapoti watumishi wa Mungu lakini ni aibu kubwa kwetu kuona kwamba mchungaji wa kanisani kwako badala ya kwenda kwenye maombi anaenda kwenye vibarua kwa sababu hana chakula. Kwa nini watu wa Mungu mnasahau watumishi wa Mungu ambao wanakesha kwa ajili ya roho zenu? Hao watatoa hesabu siku ya mwisho, sasa kama msipowapa chakula na mahitaji mengineyo mnataka waende kwenye vibarua? Mambo haya hayapaswi kuwa hivyo wapendwa hata kidogo. Nawasihi mbadilike kabisa ili kuweze kujenga ufalme wa Mungu.

Ndipo: akamwambia Mungu amkumbuke kwa hilo (13:14)

 • Alikomesha uvunjaji wa Sabato (13:15-20)

App: kuna watu wengi sana siku hizi wanasema kwamba Sabato ilishavunjwa kwa sababu hiyo hakuna cha Sabato. Na ndio maana unakuta mpendwa anaenda kwenye ibada asubuhi na akishatoka kwenye ibada anaenda KUFUNGUA DUKA LAKE! Ukitoka kwenye ibada na kwenda kufungua duka hiyo ni dhambi ya kuvunja siku ya Bwana. Kwa namna moja au nyingine katika siku ya Bwana tunaweza kufanya kazi zile ambazo hazitupi faida sisi bali zinamwinua Mungu na kuitenga siku hii kuwa maalum. Kwa mfano katika siku ya Jumapili ukimaliza ibada-tembelea kama kuna wagonjwa! Tembelea wapendwa ambao pengine hawakuja kanisani siku hiyo! Lakini si kwenda kwenye biashara au kwa ajili ya kupata faida fulani. Ninamkumbuka mama mmoja alikuwa “hatoi pesa yoyote siku ya Jumapili” na kweli ameendelea na msimamo huo mpaka leo. Kama ukimwomba hela siku ya Jumapili hatoi kabisa. Hebu ndugu zangu turudi kwenye msingi! Sababu siyo ile SIKU ni yale majukumu ambayo Mungu ametutengea katika siku hiyo.

Ndipo: akamwambia Mungu amkumbuke kwa hilo pia (13:22)

 • Aliwakemea waliooana na watu wa mataifa mbalimbali ambayo Mungu alikuwa amewakataza kuona nayo kwa sababu watawaongoza kutenda dhambi (13:23-27)

Ndipo: Neno la mwisho la Nehemia ni “Nikumbuke Mungu wangu kwa mema”

App: nafikiri sasa umeshapata picha kamili ya kile ambacho Nehemia alikifanya na ndiyo maana akawa na ubavu wa kumwambia Mungu “nikumbuke”. Mara kwa mara nimesikia maombi ya wapendwa wakimwambia Mungu “nikumbuke, je ni kwa kazi gani?”

Inawezekana kukumbukwa katika ufalme wa Mungu kama yule mwizi pale msalabani alipomwambia Yesu “Bwana nikumbuke katika ufalme wako” kwa sababu ya kukiri kwamba yeye ni Bwana, lakini maisha yako ya hapa duniani yatakuwa ni maisha ya uchungu tu kila siku.

Mwisho: naamini kabisa umejifunza mambo mengi kupitia somo hili. Sasa naomba ujibu swali langu, je UMEFANYA NINI ILI MUNGU AKUKUMBUKE? acha kusema kwamba huwezi kufanya kitu chochote kanisani! ni mawazo mabaya sana hayo.

Hebu leo fanya kitu kwa ajili ya kanisa ili Mungu akukumbuke.

Mungu akubariki sana! karibu tena ibada nyingine kama hii wiki ijayo

 

Mch. Daniel John Seni

senishekinah@gmail.com