Mizaha kwenye ibada inaweza kuleta maangamizi

Mizaha Kwenye Mambo ya Ibada inaweza kuleta Maangamizi makubwa

Kama kweli wewe umeokoka, basi ni muhimu kusoma kwa makini na kusikiliza ujumbe huu ambao Mungu anataka kuzungumza pamoja nawe siku ya leo. Kuna wakristo wengi sana ambao huwa hawazingatii mambo ya ibada ambayo Mungu ameyaagiza katika neno lake-na badala yake wanachukulia suala hili kama ni desturi tu kwa kwenda kwenye ibada kila Jumapili. Nataka nikukumbushe mambo haya mtu wa Mungu, unapokanya mlango wa kanisani tu-tayari umeingia sehemu nyingine kabisa ambayo; haitaki mizaha, utani, mbwembwe-ni sehemu ambayo Mungu anataka kufanya uthihirisho wa nguvu zake kwa waabuduo halisi. Lakini liko tatizo la watu wengi kusema kwamba hawajui wafanye nini katika ibada! Ama kwa hakika watu hawa wanahitaji kufundishwa kumtii na kumsikiliza Mungu katika nyumba za ibada.

TEXT: WALAWI 10:1-3

kitabu cha Mambo ya Walawi kama ingekuwa ni kwenye kampuni tungekiita  “job description” ya watumishi wa kampuni hiyo. Walawi inazungumzia mambo ya msingi ambayo Walawi-miongoni mwa kabila la Wana wa Israel ambalo Mungu alilichagua liweze kufanya kazi za Kiibada mbele za Mungu. Na baadaye tunaona Mungu anashughulika na familia moja ndani ya ukoo wa Lawi na familia hiyo ni ya Haruni. Katika kitabu hiki Mungu anawaeleza kwa mapana sana mambo ambayo makuhani na Waisraeli kwa ujumla wanahitaji kuyafanya hasa wanapokuwa katika ibada mbele za Mungu. Mungu aliwapa maelekezo ili wasimtende dhambi hasa wanapokuwa wako katika ibada mbele zake. Na hasa katika shughuli ya utoaji wa sadaka mbele za Mungu (yaani madhabahuni).

Kama nilivyosema hapo juu kwamba Makuhani pekee (ambao ni wana wa Haruni) ndio waliokuwa na kibali cha kuendesha mambo ya ibada. Wakati huo kama wakifanya kosa kidogo tu, Mungu anakuchukulia hatua wakati huo huo.

Katika fungu la leo tunaona Kuhani Haruni anapoteza watoto wawili kwa mpigo! Nababu na Abihu-vijana ambao walikuwa hata bado hawajaoa (lakini walikuwa watu wazima)- vijana hawa walikosema kitu mbele za Mungu siku ile walipokuwa wameenda kwenye ibada mbele zake. Ngoja turudi nyuma kidogo;

Ukisoma katika sura ya 9:22-24 tunaona mambo ya msingi sana ambayo yanaweza kutusaidia kuelewa somo hili. Tunaona hapo kuwa HaronI alikuwa ametoa sadaka ya kutekekezwa (9:12) na baadaye katika 22-24 Mungu anaikubali sadaka hiyo na moto unashuka kutoka mbinguni na kuila ile sadaka!  Biblia inasema “moto ukatoka hapo mbele za Bwana na kuiteketeza sadaka ya kutekekezwa” (v24) lakini fungu tulilosoma leo  kwamba tunakutana na maneno yaleyale lakini mwishoni ni tofauti! Yaani kinachotekezwa siyo sadaka tena bali ni watu (Nadabu na Abihu) hebu tusome hapo (10:2) “moto ukatoka hapo mbele za BWANA na ukawala (badala ya kuila ile sadaka) nao wakafa mbele za Bwana” hapa ndipo somo letu linapoanzia sasa!

Ni hakika kwamba Mungu alikuwa amemchagua Haruni pamoja na ukoo wake kwa ujumla kuwa makuhani (tena anasema milele) lakini vijana hawa kuna makosa walifanya wakati wa kutoa sadaka ambapo Mungu aliwaadhibu palepale!

Kwa nini Mungu aliwapa adhabu kali hivi vijana hawa ambao pengine wangeonywa na kutorudia tena kosa? Jibu linaweza lisiwe la moja kwa moja, lakini mojawapo ya majibu ni kwamba “Makosa ya kiibada mbele za Mungu ni makubwa mno-ni lazima tujua hili siku y aleo. Ndiyo, ni kweli  Biblia haijasema moja kwa moja sababu lakini tunaweza kufikiri kwa kurejelea baadhi ya vifungu vya Biblia.

  1. 1.     Walitoa moto wa kigeni mbele za BWANA ambao hakuwaagiza. 10:1b)

Swali la msingi hapa ni moto wa kigeni ndo kitu gani?

  1. Inaonekana kwamba walichukua moto nje ya madhabahu (16:12) tunaposoma hapa tunaona kwamba hawakutakiwa kuchukua moto kutoka sehemu nyingine yoyote ile zaidi ya madhabahuni –ambao uliwaka wakati wote. Lakini tukisoma 1:7 tunaona kibali chao cha kuwasha moto katika madhabahu, (soma). Kwa vyovyote vile vijana hawa walienda kinyume na sheria ya utoaji wa sadaka. Lakini pia kwa nini pia vijana hawakuwa makini kwa jambo hili muhimu mbele za Bwana?

Jambo muhimu hapa ni nini? “BWANA hakuwaagiza” hakuna kitu ambacho kinamkera Mungu kama kushindwa kusikia kile ambacho ametuagiza! Yaani sauti ya Mungu kabisa imekuja kwako aidha kwa kuisikia wewe mwenyewe au kwa kuletewa na nabii wa Mungu- na ukizingatia suala linahusu ibada Mungu lazima aadhibu tu.

Unakumbuka wapi ukisoma hapa? Tusome 2 Samuel 6:6-7 tunaona hapa mtu anaitwa Uzza. Huyu alifanya makosa ya kiibada pia- (kwa sababu sanduku la Agano lilikuwa kwa ajili ya ibada tu). Watu waliokuwa wanaruhusiwa kuligusa sanduku la Bwana ni makuhani peke yake-kwa sababu Uza hakuwa kuhani, Mungu alimpiga palepale na kufa!  Tukio hili linashahibiana kabisa na la hawa vijana wa Haruni. Kitu ambacho Mungu hajakiagiza ni marufuku kukifanya katika ibada.

  1. Inaonekana pia labda walikunywa vileo ambapo Mungu alisema wanakuja mbele zake wasilewe kwa kitu chochote (10:9)-tunaona agizo hili linafuatia mara baada ya tukio la kuuawa kwao mbele ya Mungu.

App. Neno linasema tusilewe kwa mvinyo ambamo mna ufisadi bali mjazwe Roho Mtakatifu. Mkristo anaruhusiwa kulewa Roho Mtakatifu tu siyo kwa kulewa pombe na madawa ya kulewa.

  1. 2.     Hawakumtukuza Mungu katika ibada yao. (v.3)

 Kwa sababau wao walikuwa wanakaa mbele za Mungu na walikuwa wametengwa kwa ajili ya kazi maalum mbele ya madhabahu. Hatujui ni heshima ya namna gani ambayo walimkosea Mungu lakini inaonekana ni makossa ya pale juu yalimvunjia Mungu heshima. Mungu aliwaweka wakfu kwa ajili yake mwenyewe Haruni na wanawe kwa kutiwa mafuta matakatifu (angalia Walawi 8:10; Walawi 8:12),ili watende kazi maalumu ya kuwa wapatanishi kati ya Mungu na mwanadamu. Lakini baada ya kushindwa kufanya hivyo, Mungu alijitakasa mwenyewe ndani yao kwa adhabu kali na ya kwa sababu ya makosa yao.

ð      Mungu alikasirika sana baadaye kwenye ukuhani wa Eli (1 Samuel 2:29-30) kwa sababu vijana wale walishindwa kumheshimu Mungu kabisa-Mungu alikusudia kuwaua kimwili na kumfukuza Eli katika ukuhani wake.

ð      Mungu haangalii sura ya mtu. Hebu ngoja nikukumbushe habari za Musa na Haruni huko mbele ya safari walijichanganya Mungu akawa suspend haraka sana.  Tusome  Hesabu 20:7-8 “Mungu alimwambia uambie mwamba utoe maji” lakini Musa kwa sababu ya mazoea badala ya kufuata maelekezo 20:11 akaupiga ule mwamba tena mara mbili! Sasa sikiliza msitari unaofuatia hapo “Mungu akawaambia Musa na Haruni kwa sababu hamkuniamini mimi wala hamkuniheshimu mbele ya mkutano-basi kutano hili hamtaliingiza katika nchi niliyoahidi” (v12). Hapa Mungu akafunga kazi. Hii kitu ilimtesa sana Musa na anasema kwamba alimwomba Mungu sana amsamehe lakini aligoma! (Soma Kumb. 3:23-26)

ð      Wewe umetengwa kwa ajili ya kulitangaza-ukimheshimu Mungu yeye atakuheshimu

Katika adhabu hii Mungu alikuwa akitoa onyo kali na makuhani wengine wote ambao wangetumika katika hema yake, na baadaye, katika hekalu pia.

 Mungu alifanya hivyo pia kwa sababu hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwao kutoa sadaka katika ya kuteketezwa kwa hiyo alitaka aanze na funzo hilo.

Mara kwa mara Mungu hutoa adhabu kali kwa watu wanaoshindwa kumheshimu yeye katika ibada za aina mbalimbali. Kutoa sadaka ni ibada! Hebu tuangalie tukio moja baya katika  Matendo  5: 1-11, wakati wa muda wa kanisa la kwanza. Anania na Saphira walipotenda kosa kama hili Mungu aliwahukumu kifo cha kimwili palepale! Kwa sababu walifikiri wanasema uongo kwa Petro lakini kumbe ilikuwa kwa Mungu. (Matendo 5: 4). Petro alisimama mahali pale katika ibada kwa niaba ya Mungu-kwa hiyo tukio lolote lililoenda kinyume na Mungu lilihesabika kuwa uvunjaji wa sheria na kumkosea Mungu heshima.

App: yawezekana hutoi zaka kabisa na badala yake unawadanganya watumishi wa Mungu kwamba unatoa-na wengine wameacha kutoa zaka na badala yake waandika shukrani!!! Weweweweeeee-usimtanie Mungu! Mungu si wa kutaniwa~unajitafutia matatizo ya kiuchumi wewe mwenyewe! Unajua uchumi wako unaweza kuyumba na usijue umeanzia wapi kuyumba? Eeh? Ni kwa sababu unadhani unamdanganya Mchungaji wako-kumbe Mungu anakuchungulia na kucheka tu. Kama ukiamua kula zaka ya Mungu maana yake wewe unajiweka kwenye nafasi ya ukuu kuliko Mungu-yaani unamsaidia Mungu kutumia kilicho cha kwake! Hatari sana. Geuka leo kabla hujapata pigo.

Application: kuna ibada za namna mbalimbali ambapo watu badala ya kuheshimu Mungu humdharau Mungu kwa kufanya vitu visivyopendeza mbele za Mungu.

a)     Kwa mfano kuna watu wanaugua magonjwa ya kimwili kwa sababu ya kushiriki ibada ya meza ya Bwana (1 Kor 11:28-30). Kuwa makini mtu wa Mungu unapokuwa katika ibada. Usichukulie kila kitu kuwa ni poa ndani ya nyumba ya Mungu.

b)     Kuna watu maisha yao ya kimwili yanaashiria kwamba kiroho chao hakiko sawa kwa sababu walimkosea Mungu wao. Kuna vijana wengi sana leo wanajidai kuwa ni wataalam wa kutenda dhambi (na wanajisifu-wanatembea na wanakwaya kila kukicha-hata wakimaliza ibada wanaenda kufanya uzinzi-hao watu wanaweza kufa kifo kibaya sana).

c)     Kaka zangu, dada zangu, hebu tuache mchezo tunapokuwa katika ibada mbele za Mungu! tuacheni mizaha katika ibada-takatifu kwa sababu madhara yake ni makubwa sana.

d)     Waabuduo halisi “Watamwabudu baba katika Roho na Kweli-Mungu ni Roho-nao wamwabuduo imewapasa kumwabudu katika Roho na Kweli. Tafadhali unapokuja mbele za Mungu katika ibada kaa katika uwepo wake-tafakari neno lake-ombe kwa nguvu zote-

Onyo: ndani ya ibada siyo sehemu ya kusalimiana! Ndani ya ibada ni sehemu ya kusikiliza maelekezo ya Kimungu kwa siku hiyo. Hebu nenda na matumaini katika ibada ya kupata kile ambacho Mungu anataka kukuelekeza kwa siku hiyo. Acha kwenda kwenye ibada kwa sababu ya mchungaji wako atakuonaje usipoenda. Unajua ndiyo maana tunao watu ambao si maskini na wala si matajiri (kwa sababu wao wako vuguvugu). Haya yanaweza kuwa ni matokeo ya kutokumwabudu Mungu vizuri moyoni mwako.

 Naomba Mungu akufundishe na kukuepusha kufanya mizaha mbele zake unapokuwa katika ibada.