PAMBANA NA ROHO YA KUKATALIWA KABLA MUNGU HAJAKUKATAA

TITLE: PAMBANA NA ROHO YA KUKATALIWA MAPEMA KABLA MUNGU HAJAKUKATAA

FUNGU: SAMUEL 15:23

Hili somo ni muhimu sana kwako wewe ambaye unayetaka maendeleo ya kimwili na kiroho! Katika maisha ya hapa duniani, kuna vitu vingine ambavyo sisi kwa upande wetu tunapaswa kuvifanya kwa nguvu zote-lakini kuna vitu vingine ambavyo ni vya upande wa Mungu. Mwanadamu hushirikiana na Mungu katika kutimiza makusudi yake hapa duniani. Mungu hafanyip peke yake kuhusu hatima ya mwanadamu- bali anashirikiana na mwanadamu. Kwa nini anashirikiana naye? Mwanadamu aliumbwa kwa mfano wa Mungu (kwa hiyo mwanadamu anao mfano wa Mungu-si kwa sura bali ni akili na ufahamu wake). Na pia mwanadamu anaweza kumfahamu Mungu kwa sehemu (ingawa hawezi kumfahamu kwa 100%-lakini kwa namna Fulani anaweza kumfahamu) kwa sababu Mungu mwenyewe amejifunua kupitia 1. Uumbaji wake 2. Kwa kumleta Yesu Kristo aliyekuja kwa umbo la mwanadamu.

Kwa hiyo binadamu anapaswa kuchakarika usiku na mchana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba upande wake unatimiza majukumu kikamilifu. Kuna vitu vya msingi ambavyo unapaswa kuvielewa unapokutana na fungu hili

a)     Waisrael walipoingia Kanaani hawakuwa na mfalme (yaani maana yake ni kwamba hajakuwepo mfalme wa kidunia kwa Waisrael tangu watoke Misri mpaka kufikia hatua hii)

b)     Waisrael walimwomba Mungu wapate mfalme ili wafanane na watu wa mataifa mengine (yaani walifanya jambo ambalo lilihusu upande wao) lakini upande wa Mungu haukupendezwa kwa sababu kufanya hivyo ilikuwa ni kumfanya Mungu kama siyo kiongozi wao na hivyo walitamani kuwa kama watu wa duniani.

Lakini baadaye tunaona Mungu anaridhia maombi yao na anamchagua Sauli kama mfalme wa kwanza wa Israel.

Lakini kuna roho hapa ambayo mimi nasema Sauli hakuishughulikia mapema na kama angeishughulikia mapema pengine isingeleta matatizo baadaye.

Tusome 1 Samuel 10:27 Biblia inasema “lakini wengine wasiofaa kitu wakasema, Huyu je atatuokoaje? Nao wakamdharau, wasimletee zawadi” lakini hapa kwa mbele yake Tafsiri yetu ya Kiswahili ina changamoto kidogo, waliruka kipengele muhimu sana ambacho kinasema(“but Saul kept silent” )“lakini Saul alinyamaza” (ni changamoto ya kawaida, ndio maana umekuja kanisani kujifunza na vinginevyo usingeelewa)

Hii ilikuwa ni siku ya utambulisho wa Sauli kuwa mfalme wa Israel ambapo tunaona kwamba kundi kubwa la wana wa Israeli lilimuunga mkono (10:24) lakini kundi dogo la watu wasiofaa- (troublemakers) wakamdharau. Hii ilikuwa ni roho mbaya iliyokuwa inaenda kinyume na utawala wa Sauli. Na hili kundi dogo ambalo mwandishi anatuambia kwamba ni kundi la watu wasiofaa-walianza kuhoji mapema kabisa ni kwa namna gani Sauli atawaokoa kutokana na mikono ya adui zao (hasa Wafilisti).

Wakati mwafaka wa kulishughulikia kundi hili Sauli aliupata (soma 11:12-13) “Ndipo watu walipomwambia Samweli, ni nani yule aliyesema, Je huyu Sauli atatutawala (reign over us)? Walete watu hao, ili tuwaue, Lakini Sauli akasema Hakuna mtu atakayeuawa leo, maana leo BWANA amefanya wokovu katika Israel

Hatusomi mahali popote kwamba Sauli aliwaua hawa jamaa! Katika kipindi kile kumshughulikia mtu aliyeenda kinyume nawe ilikuwa ni sahihi kabisa kwa sababu lilikuwa ni suala lililohusu ufalme. Cha kushangaza sana, Sauli baada ya kuona mambo yanakuwa magumu akaanza kumsaka kijana wa watu Daudi ili amuue eti kisa anataka kuridhi ufalme wake. Mimi sikwambii ukaanze kutafuta watu uanze kuwachinja lakini ninachosema ni muhimu mno kushughulikia jambo linapokuwa linaanza. Upinzani unapokuwa unaanza ni lazima uushughulikie- hata hivyo kuna upinzani mwingine ambao unaletwa na Mungu kwa ajili yako kama usipojua hata kama ukipinga haitasaidia. Kwa mfano Herode alishughulikia mapema sana upinzani wake kutoka kwa Yesu na akaanza kutafuta kumuua Yesu lakini mwisho wake aliishia kuua watoto ambao hawakuwa na hatia hata kidogo.

Hata hivyo unaweza kuona namna ufalme wa Sauli ulivyokuwa na changamoto nyingi sana. Swali je, hayo maneno ya watu wasiofaa yalikuwa yana ukweli au hayana ukweli? Kulikuwa na ukweli ndani yake. Ingawa ni mstari mmoja lakini tukiangalia utumishi wa Sauli kwa ujumla kundi hili la watu wachache ambao tena hawafai lilikuwa na ukweli ndani yake. Ushahidi huu hapa:-

a)     Sauli alishindwa kumuua Goliathi- (1 Sam.17) jambo hili lilileta dharau kubwa mno kwake. Kwa sababu hiyo kauli ya hawa jamaa ilikuwa na ukweli ndani yake. Yaani jeshi zima la Israeli limeogopa kwenda kumpiga mtu mmoja tu ambaye alikuwa anayatukana majeshi ya Mungu! Daudi alimshambulia mara moja Goliathi na kufa.

b)     Sauli alichelewa kuishughulikia mapema roho hii mpaka watu wakahamishia mapenzi yao kwa Daudi (soma 1 Sam 18:7-8) biblia inasema “Sauli akagadhibika sana, na maneno hayo yakamchukiza.

App: Yawezekana unaona watu wengi wanakusapoti na unapoliona kundi dogo la watu wanaokupinga hutaki kulishughulikia na kuondoa upinzani wao-nataka nikwambie kwamba kama wewe ni mwanasiasa-utashuka vibaya sana. Kama wewe ni mtumishi na umevuma kila mahali-utashuka sana.

Unajua? Watu wengi wanapokuwa wanakusapoti katika mawazo yako na katika kazi zako unainua kiburi moyoni mwako-unajiona kwamba hawa watu wote wanaoniunga mkono kweli kuna siku wataniacha? Kama hujui-kamuulize Sauli siku aliposikia wanawake wametunga nyimbo za kumpongeza Daudi badala ya mfalme.

Ndiyo? Shughulikia mapema kama kuna roho ya kundi dogo linaloenda kinyume na wewe ili ujue kwa nini liko kinyume? Pengine kundi hilo lina hoja malidhawa! Si kila anayekupinga ni adui yako-mwingine ana lengo la kukusaidia.

c)     Alishindwa kushughulikia mawazo hasi kuhusu yeye (1 Samuel 10:10-11) unajua watu walizusha usemi “je Sauli naye ni miongoni mwa manabii” huu usemi katika lugha ya Kiebrania unaonesha dharau! Yaani wewe huwezi kuwa “mtu fulani.”

Je unafikiri Sauli angeshughulikiaje tatizo hili? Ni kweli alikuwa na uwezo wa kutuma jeshi lake na kuwaangamiza wote walikuwa wanamdharau. Lakini ile siyo! Na kweli hakufanya hivyo.

  1. Alitakiwa kuonesha mfano tofauti na watu walivyofikiri juu yake (yaani alipaswa ajitahidi ili wale wanaosema hawezi waone kwamba anaweza kuliko mawazo yao) alitakiwa aokomae pamoja na Mungu
  2. Alitakiwa amtii Mungu na kufuata mapenzi ya Mungu na hapo hayo maneno ya dharau kutoka kwa washindani wake yangekoma.

App: Leo nakusihi ugundue ni akina nani wako kinyume nawe? Katika  kitabu cha Nehemia tunagundua kwamba Nehemia aliwagundua maadui zao (Tobia na Sanbalati-walikuwa wanavicheko vya dharau kwao) na Nehemia aliamua kumtii Mungu peke yake. Na matokeo yalionekana!

d)     Sauli hakumsikiliza Mungu-angewezaje kuwaokoa watu hawa. Mungu alimwambia akawapige Waamaleki na kumaliza kila kitu (1 Sam. 15ff) lakini badala yake alichukua mateka kondoo, ng’ombe na vitu vingine (mst 20), kwa hiyo badala ya kuisikiliza sauti ya Mungu akasikiliza sauti za wanadamu. Tunaweza kusema kuwa watu hao hao walimsapoti kipindi cha nyuma ndi hao hao waliopotosha na akawasikiliza walipoona kuna mali ya kuteka nyara!

Mungu anataka nini? Mungu anataka utii tu kwa kile ambacho anatuagiza, yaani kutembea katika njia zake. Kutembea mbele zake. Sisi ni wanadamu, hatuko wakamilifu-lakini kutii kile ambacho Mungu anakata kitekelezwe wakati huo ni muhimu mno.

Matoke ya tukio hili nini? Mungu alimkataa Sauli asiwe mfalme wa Israel! Ni lazima uishughulikie hii roho mapema sana kabla Mungu hajatia mkono wake hapo.

Mungu akikukataa:-

a)     Hakuna nabii anayeweza kukuombea (1 Sam.16:1), Mungu alimpiga stop Samuel kuendelea kumwombea Sauli kwa sababu Mungu alikuwa amemkataa.

b)    Musa alipigwa stop asiendee kuomba tena kibali cha kufika Kanaani ( Kumb.3:26 “Bwana alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize Bwana akaniambia; Na ikutoshe, usinene nami Zaidi jambo hili” kama Musa ilifikia hatua akazuiwa! Mtu ambaye alikuwa ana uwezo wa kutuliza hasira ya Mungu aliyetaka kuwaangamiza Waisrael wote lakini kwa sababu yake Mungu alikubali kuwasamehe! Wewe ni nani?

Mwisho: narudia kusema, pambana na roho ya kukataliwa mapema kabla Mungu hajakukataa

Ameni